Tuesday, January 8, 2008

JINSI YA KUISHI NA MTU MWENYE UGONJWA WA KIFAFA

Karibuni tena wapenzi wasomaji katika makala hii ya Daktari wako.Jumapili ya leo tutaangalia jinsi ya kuishi na mtu mwenye kifafa kwa kutazama dalili za awali,vigezo hatarishi,uchunguzi uambatanao na ugonjwa wa kifafa na hatua za kuchukua iwapo mtu amepatwa na kifafa.

Utangulizi
Ubongo wa binadamu umeundwa na zaidi ya seli za neva (seli za fahamu) bilioni mia moja.Seli hizi zote huwasiliana ambapo baadhi huzichokoza nyingine kutuma jumbe zaidi wakati nyingine huzifanya nyingine kutotuma ujumbe kama inavyotakiwa.Utendaji mzuri wa ubongo unategemea uwiano katika kutuma ujumbe.Utumaji usio na udhibiti hupelekea mlipuko wa umeme katika seli za ubongo ambapo huweza kupelekea mtu kupata kifafa (seizure) hali ambayo huambatana na kupoteza fahamu,kuzubaa,kukakamaa misuli,kuchanganyikiwa au kuchezesha viungo haswa mikono na miguu.
Sote tuko katika hatari ya kupata kifafa.Kifafa chaweza tokea bila sababu dhahiri lakini watu waliowahi kudhurika ubongo wako katika nafasi kubwa ya kupata kifafa. Kifafa hakirithiwi ingawa mara chache hutokea hivyo na zaidi haswa kwa ndugu ambao wana muathirika wa kifafa.

Aina za Kifafa
Kuna aina kuu mbili za kifafa,nazo ni Kifafa Kamili (Generalised seizure) na Kifafa Upande (Partial seizure).
Kifafa Kamili (Generalised seizure)
Kifafa cha aina hii huwa na milipuko ya umeme katika seli za fahamu za ubongo mzima au sehemu kubwa ya ubongo.Aina hii ya kifafa huambatana na kupoteza fahamu.
Kifafa Upande (Partial seizure)
Katika aina hii ya Kifafa sehemu tu ya ubongo huwa imeathirika.Dalili hutegemea sehemu husika ya ubongo iliyodhurika.Si kawaida kwa waathirika wa aina hii ya kifafa kupoteza fahamu.Waathirika wake hupatwa na mishtuko ya misuli haswa mikono na miguu.
Vigezo hatarishi vya mtu kupata kifafa
Vifuatavyo ni baadhi tu ya vigezo hatarishi ambavyo vyaweza kupelekea mtu kuathirika na ugonjwa wa kifafa:
-Watoto waliozaliwa njiti
-Watoto wapatao kifafa katika mwezi wa kwanza mara tu baada ya kuzaliwa
-Kuvujia damu kwenye ubongo
-Kuwa na mishipa yenye matatizo kwenye ubongo
-Madhara makubwa kwenye ubungo
-Ukosefu wa hewa ya oksijeni ya kutosha kwenye ubongo
-Saratani ya ubongo
-Magonjwa yanayoathiri ubungo kwa mfano homa ya uti wa mgongo
-Kiharusi
-Historia ya kuwepo kwa kifafa au degedege liambatanalo na homa katika familia
-Utumiaji wa dawa za kulevya kama kokeini
-Madhara ya wastani kichwani na kupoteza fahamu kwa muda

Sababu zipelekeazo mtu kupata kifafa
Kwa zaidi ya theluthi mbili ya wagonjwa wa kifafa hakuna sababu maalum iliyogundulika ila kitendo cha historia ya uwepo wa kifafa kwenye familia inaashiria kuwepo kwa sababu za kijenetiki.
Sababu zifuatazo pia zinahusishwa:
-Madhara kwenye kichwa
-Operesheni ya kichwa
-Magonjwa ya ubongo kama homa ya uti wa mgongo
-Kiharusi
-Saratani ya ubongo
-Unywaji pombe wa kupindukia
-Kupungua chini ya kiwango kwa sukari katika damu (hypoglycemia)
Pia mpendwa msomaji ni vyema ukafahamu vitu ambavyo vinaweza kuchokoza kifafa.Hivi si vingine bali ni:
-Mwanga mkali kama wa flashi ya kamera, taa ya gari, runinga n.k
-Homa kali
-Msongo wa mawazo na kutolala
-Kilevi
-Dawa za kulevya kama kokeini, heroini n.k
-Homoni.Wakati estrojeni zinapokuwa juu au projestroni kushuka.Hii yaweza kutokea siku chache kabla ya kuingia kwenye hedhi au wakati wa hedhi au wakati wa kutolewa kwa yai (ovulation).
-Madawa haswa yale ya magonjwa ya akili
-Upungufu wa virutubisho (nutritional deficiencies)
Dalili za mwanzo za tahadhari za kifafa
-Kutoona vizuri
-Kujisikia vibaya/ kiajabuajabu
-Kuogopa
-Kizunguzungu
-Kichefuchefu
-Kusikia kama vitu vikikutambaa mwilini
-Kusikia ganzi
Hata hivyo kifafa chaweza kuja bila dalili za wawli za tahadhari.Dalili zifuatazo zaweza tokea:
-Kupoteza fahamu kwa ghafla (black out)
-Kuchanganyikiwa
-Kuzimia
-Kupoteza uwezo wa kuona
-Woga
-Kutafuna tafuna ulimi
-Kupata shida ya kuongea
-Kutoa mate
-Kuviringisha macho
-Kudondoka
-Kutupa tupa miguu
-Kupunga mkono
-Kushindwa kujizuia haja (kubwa/na ndogo)
-Kushindwa kusogea
-Kujilamba midomo
-Kuduwaa
-Kukakamaa
-Kutoa jasho
-Kutetemeka
-Kupumua kwa shida
-Kubana /kusaga meno
-Moyo kwenda mbio
Baada ya kifafa wagonjwa wa kifafa huwa na dalili zifuatazo:
-Kupoteza kumbukumbu
-Kuchanganyikiwa
-Kuwa na mfadhaiko (majonzi)
-Maumivu ya kichwa
-Kichefuchefu
-Michubuko
-Maumivu
-Kiu
-Kuchoka
-Hamu ya kujisaidia (haja kubwa au ndogo)
Nini cha kufanya iwapo mgonjwa wa kifafa amepatwa na kifafa
-Ondosha vitu vyovyote vinavyoweza kumdhuru kama moto n.k
-Usijaribu kumzuia kurusha miguu au mikono
-Usimuhamishe kumpeleka mahala pengine
-Mgeuze upande (kiubavu) ili kama kuna kimiminika chochote mdomoni kiweze kutoka
-Toa nguo yoyote iliyobana shingoni ili aweze kupumua vizuri
-Kaa naye mpaka apate fahamu (yaweza kuchukua mpaka dakika kumi na tano)
Usifanye yafuatayo:
-Kuweka kitu chochote mdomoni
-Kujaribu kumzuia mgonjwa asirushe mikono au miguu

Uchunguzi
Vipimo vifuatavyo ni muhimu kutokana na uwezo wa mgonjwa katika kugundua chanzo cha tatizo kwenye ubongo kiletacho kifafa:
Kipimo cha Kompyuta cha Kuchunguza ubongo (CT Scan);Kipimo hiki huonyesha sehemu mbalilmbali za ubongo kuchunguza kama kuna athari yoyote.
Kipimo kingine ni cha electroencephalogram (EEG) ambacho husaidia kufuatilia hali ya utendaji wa kiumeme wa seli za ubongo.
Kipimo kingine cha uhakika zaidi lakina aghali ni cha kuchunguza ubongo kwa usumaku Magnetic Resonance Imaging (MRI).
Matibabu na Ushauri
Ni vyema kumuona daktari aliye karibu nawe iwapo una tatizo au una mtu mwenye tatizo la kifafa.Kumbuka mtu mwenye kifafa anaweza kuishi maisha ya kawaida kama mtu mwingine iwapo atadhibiti dalili na kunywa dawa kama alivyoelekezwa na daktari.Hakikisha unafuata maelekezo ya daktari wako kuhusu matumizi ya dawa na epuka kuacha kunywa pombe wakati ukiendelea na matibabu.Endelea na matibabu hata pasipo na dalili, wasiliana na daktari wako kabla ya kuacha kutumia dawa.Pia ifahamike kwamba kifafa si ugonjwa wa akili na si ishara ya kuwa na uwezo mdogo kiakili.
____________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 4 Novemba 2007)
______________________________________________
UGONJWA WA PUMU (ASTHMA)

Karibuni tena wapenzi wasomaji wa safu hii ya Daktari wako.Jumapili ya leo tutaangalia Ugonjwa wa pumu au asthma kama ujulikanavyo kwa lugha ya kitaalamu.

Ugonjwa huu si mgeni miongoni mwa watu wengi na ni dhahiri ama tumeshawahi kumwona au kuishi na mgonjwa wa pumu kama siyo baadhi yetu kuugua ugonjwa huu.

Utangulizi

Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu ambao huathiri njia za hewa ambazo huingiza na kutoa hewa katika mapafu.Upatapo ugonjwa wa pumu, kuta za ndani za njia ya hewa hupata maumivu (inflammation) na kuvimba.

Maumivu katika njia za hewa huzifanya kujihami kwa kusinyaa na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachopita kwenda kwenye mapafu.Hali hii husababisha muathirika kutoa mlio kama wa filimbi au mluzi wakati wa kupumua.
Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu lakini unaotibika.Unaweza kudhibitiwa kama vile ugonjwa wa kisukari na moyo unavyoweza kudhibitiwa.

Aina za Pumu

Kuna aina kuu mbili za pumu.Aina ya kwanza ni ile inayoanza mapema (early onset asthma) na aina ya pili ni ile inayochelewa kuanza (late onset asthma).Kwa kifupi tutaenda kuangalia tofauti chache kati ya aina hizi za pumu.

Pumu inayoanza mapema
Ni kawaaida kwa aina hii ya pumu huanza utotoni na kwa kawaida huwatokea waathirika ambao miili yao hutengeneza kingamwili (antibodies) za IgE.Waathirika wa aina hii ya pumu hutambuliwa kwa vipimo maalum vya ngozi ambapo huonyesha kuathirika kwa asilimia kubwa ya vipimo hivyo vinapofanywa.

Pia waathirika hawa huwa na matatizo mengine ya mzio (allergic disorders) kama mafua na ukurutu (eczema)

Pumu inayochelewa kuanza
Aina hii ya pumu,tofauti na iliyopita,huanza katika umri wowote na asilimia kubwa ya waathirika ni watu wazima.Hakuna ushahidi wowote unaohusianisha vizio (allergens) vinavyotokana na mazingira na uwezo wa kusababisha aina hii ya pumu.

Pumu husababishwa na nini?

Bila shaka mpenzi msomaji umekua ukijiuliza swali hili mara kwa mara.Haifahamiki haswa ni sababu zipi zinazopelekea njia za hewa kupata maumivu na hivyo kupelekea mtu kupata pumu.Vyanzo mbali mbali vinaonyesha kuwa ni kutokana na mseto wa vitu kama tumbaku,maradhi na baadhi ya vizio.Pia kuna vitu katika mazingira ambavyo vinaweza kusababisha mtu kushambuliwa na pumu.Vitu kama vile mazoezi, vizio, viwasho (irritants) na maradhi yatokanayo na virusi.

Baadhi ya vizio ni kama vifuatavyo:
-Vumbi
-Mende
-Chavua (pollen) kutoka kwenye miti na majani
-Magamba ya wanyama,manyoya n.k

Viwasho kama:
-Moshi wa sigara
-Uchafuzi wa hewa
-Harufu kaili (kutoka kwenye rangi au chakula)
-Msongo wa mawazo

Vingine ni kama:
-Madawa kama Aspirin
-Ugonjwa wa kucheua
-Viwasho au vizio vitokanavyo na kemikali
-Magonjwa ya njia ya hewa n.k

Ieleweke kwamba orodha iliyotajwa hapo juu siyo kamilifu kwa maana kwamba haijasheheni vitu vyote vinavyoweza kuleta dalili za pumu na pia muathirika anaweza kuathirika na kimoja wapo au zaidi.

Vigezo hatarishi
Baadhi ya vigezo hatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa kusababisha ugonjwa wa pumu ni pamoja na:
-Kuishi katika miji mikubwa,haswa katikati ya mji ambapo huongeza uwezekano wa kukutana na vizio
-Kuvuta hewa iliyo na moshi
-Kemikali zitokanazo na kilimo,dawa za kutengeneza nywele, rangi, vyuma, plastiki au vifaa vya elektroniki
-Kuwa na mzazi mmoja au wawili wenye pumu
-Kuathirika na maradhi ya mfumo wa hewa kama kikohozi na mafua wakati wa utoto
-Unene wa kupita kiasi (obesity)
-Ugonjwa wa kucheua na kiungulia (Gastro esophageal reflux disease)

Dalili za Pumu

Baadhi ya dalili za kawaida za ugonjwa wa pumu ni kama zifuatazo:
-Kikohozi: Mara nyingi kikohozi cha pumu huwa kikali nyakati za usiku au alfajiri na hivyo kumfanya mwathirika kutolala vizuri
-Kutoa sauti ya mfano wa mtu anayepiga mluzi au filimbi wakati wa kupumua
-Kifua kubana: Mgonjwa husikia kama kitu kinakandamiza kifuani au wakati mwingine husikia kama mtu amemkalia kifuani.
-Kukosa hewa: Baadhi hujisikia kama hawawezi kupukmua na kukosa hewa ya kutosha inayoingia au kutoka kwenye mapafu
-Kupumua haraka haraka

Ikumbukwe kwamba si watu wote huwa na dalili zilizokwisha tajwa hapo juu na dalili zaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.
Dalili pia zaweza tofautiana ukali.Wakati mwingine dalili zaweza kuwa za wastani,za kukera tu au mbaya kiasi cha kumzuia muathirika kufanya shughuli zake za kila siku.Vile vile dalili zaweza kuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha.
Dalili pia zaweza kutofautiana kwa kipindi zinapotokea.Wengine hupata dalili mara moja tu kwa mwezi,wengine kila wiki na wengine hupata dalili kila siku.Hata hivyo iwapo muathirika atapata matibabu sahihi anaweza kuishi na dalili chache au bila dalili kabisa.

Uchunguzi

Kipimo cha muhimu katika uchunguzi iwapo mtu ameathirika na pumu ni kuangalia jinsi mapafu yanavyofanya kazi.Kipimo hicho kijulikanacho kwa lugha ya kitaalamu kama spirometry hutathmini kiasi cha hewa mtu waezacho kukitoa baada ya kuvuta hewa kwa nguvu na kwa haraka kiasi gani.
Viwango huwa chini ya kawaida iwapo njia za hewa zina maumivu na zimesinyaa.
Kipimo hiki cah spirometry pia hutumika kutathmini jinsi mgonjwa wa pumu anavyoendelea,kupata nafuu au tatizo kuongezeka.
Hata hivyo kipimo hiki ni kwa ajili ya watoto wenye zaidi ya miaka mitano na watu wazima tu.

Baadhi ya vipimo vingine vinavyoweza kiufanywa iwapo kipimo cha spirometry hakitaonyesha tatizo ni:

Kipimo cha Kizio (Allergy test)
Husadia kugundua iwapo kuna vizio mbalimbali vinavyoathiri mwili wako.

Kipimo cha Mazoezi
Kugundua iwapo kuna mabadiliko yoyote katika njia ya hewa kutokana na mazoezi.

Kipimo cha Ugonjwa wa Kucheua na Kiungulia
Kipimo hiki ni muhimu pia kutokana na uhusiana uliopo kati ya kiungulia,kucheua na ugonjwa wa pumu.

Kipimo cha Picha ya Mapafu (X-ray)
Kipimo hiki pia chaweza kuhitajika kuona iwapo kuna kitu chochote kilichoziba njia ya hewa au kama kuna maradhi yoyote katika mapafu au moyo.


Kutokana na vipimo daktari wako atapata picha ya ukali wa pumu yako na kukuanzishia tiba muafaka.

Matibabu

Kuna aina mbili za matibabu ya pumu.Moja ni ile ya dharura ili kutoa msaada au nafuu ya haraka.Dawa hizi ni zile zinazosaidia kutanua njia za hewa ambazo zimesinyaa (bronchopdilators) pia husaidia kuilainisha misuli ya njia za hewa iliyosinyaa ili iweze kutanuka na kuruhusu hewa ya kutosha kuingia.
Ni vizuri kutumia dawa za kuleta nafuu haraka punde uonapo dalili za pumu zilizooorodheshwa hapo juu.

Aina nyingine ya dawa ni zile za muda mrefu.Aina hizi za dawa hutumiwa mara kwa mara kwa kipindi kirefu kuzuia dalili za pumu na mashambulizi.Watu wenye pumu isiyoisha wanahitaji matumizi ya dawa ya muda mrefu.Kotikosteroidi za kuvuta (inhaled corticosteroids) ni nzuri kwa aina hii ya pumu.

Matibabu ya pumu kwa watoto
Watoto wenye pumu kama ilivyo kwa watu wazima wanapaswa kumwona daktari kwa matibabu.Watoto walio na umri mdogo wanahitaji uangalizi wa wazazi/walezi ili kudhibiti pumu.Watoto wenye umri mkubwa wanaweza kujifunza wenyewe jinsi ya kutumia dawa chini ya uangalizi mdogo kutoka kwa wazazi.


Matibabu ya pumu kwa watu wazima
Watu wazima wanaweza kutakiwa kupunguza au kuongeza matumizi ya dawa za pumu kutokana na maradhi mengine waliyonayo.Madawa kama ya kutibu shinikizo la juu la damu,ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona (glaucoma),aspirini na dawa za maumivu (non steroidal anti inflammatory drugs) huingiliana na utendaji wa dawa za pumu au zenyewe kusababisha pumu.

Matibabu wakati wa ujauzito
Ni muhimu kudhibiti vyema ugonjwa wa pumu wakati wa mimba kwani iwapo utasababisha kusinyaa kwa njia ya hewa basi waweza kupelekea upungufu wa hewa ya oksijeni kwa mtoto hali ambayo ni hatari kwa mtoto.

Dawa nyingi za pumu hazina madhara kwa kichanga hivyo ni muhimu kuendelea na matibabu wakati wa mimba kuliko kuacha.

Kinga

Njia pekee ya kujikinga na pumu ni kuepuka vizio vinavyoweza kusababisha kuanza kwa dalili za pumu.Waweza fanya hivyo kwa kusafisha nymba kila wiki kupunguza vumbi,kuepuka kufanya mazoezi kwenye baridi,epuka moshi wa sigara, dhibiti ugonjwa wa kucheua na kiungulia,epuka kukaa na wanyama na epuka kuishi katika mazingira yenye hewa yenye unyevunyevu.

Ushauri

Jinsi ya kumsaidia mtoto mwenye pumu
-Mpeleke kwa daktari kwa uchunguzi wa mara kwa mara na matibabu
-Mueleweshe kuhusu pumu na jinsi ya kuidhibiti
-Mueleweshe ajue vitu vinavyoweza kusababisha yeye kupata dalili za pumu na jinsi ya kuepukana navyo
-Muepushe na moshi wa sigara kwa kutovuta sigara na kutoruhusu watu kuvuta sigara nyumbani kwako
-Tafuta jinsi ya kumpunguzia mtoto wako kukutana na vizio kama vumbi,chavua,mende n.k
-Hakikisha anatumia dawa kama inavyotakiwa
-Mhimize kufanya mazoezi ya viungo.



_________________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 9 Desemba 2007)________________________________________________________________________
UGONJWA WA SELI MUNDU
(SICKLE CELL)


Wapendwa wasomaji katika mada ya leo na kwa faida ya wasomaji wengine nitapenda kujibu baadhi ya maswali mbalimbali kutoka kwa wasomaji wa makala hii ya Daktari kwa kuuelezea ugonjwa wa Seli Mundu ambao ni ugonjwa wa kawaida katika jamii yetu ambayo imekuwa na dhana tofauti kuhusu ugonjwa huu.

Kabla ya kuanza kuuelezea ugonjwa wenyewe ni vyema basi mpendwa msomaji ukafahamu jinsi gani damu husafirishwa katika mwili wa damu.

Himoglobini (haemoglobin) ni molekyuli ambayo ni sehemu ya chembe hai nyekundu zilizoko mwilini.Himoglobini hufanya kazi ya kuzisaidia chembe hai nyekundu kubeba hewa ya oksijenu kutoka kwenye mapafu kwenda sehemu nyingine za mwili.

Kwa kawaida binadamu anapozaliwa huwa na himoglobini ya kawaida ambayo huitwa himoglobini A (Haemoglobin A) au kwa kifupi HbA na Himoglobini ya kichanga ambayo huitwa Himoglobini F (HbF).Himoglobini A ambayo hutengeneza takriban asilimia tisini na saba ya Himoglobini za mtu mzima imeundwa na jozi mbili za minyororo (chains) za alfa (alpha) na beta (beta).

Chembe hai nyekundu za damu za kawaida huwa laini,za duara na huweza kujipenyeza katika mishipa ya damu kirahisi.Pia huweza kuishi kwa takriban siku mia moja na ishirini (120) kabla chembe hai nyekendu za damu mpya hazijatengenezwa.

Watu wenye ugonjwa wa sickle cell wao huwa na chembe hai nyekundu ngumu, zenye umbo la mundu au mwezi mchanga ambazo hupita kwa shida kwenye mishipa ya damu haswa ile midogo.Aina hii ya himoglobini huitwa Himoglobini S (HbS).Tofauti na chembe hai nyekundu za damu za kawaida,zenyewe huishi kwa siku chache zaidi, kwa kawaida takribani siku kumi na sita (16) tu.

Kwa hiyo ugonjwa wa sickle cell ni ugonjwa wa kurithi ambapo mwathirika huwa na himoglobini S ambayo hupelekea chembe hai nyekundu za damu zisizo za kawaida kushindwa kupita kwenye mishipa ya damu kirahisi.Hali hii hupelekea kuwa na upungufu wa damu kwenye baadhi ya sehemu mwilini.

Hata hivyo iwapo chembe hai nyekundu za damu HbA ni zaidi ya HbS huweza kutengeneza HbAS.Hali hii hujulikana kitaalamu kama Sickle cell isiyo na dalili (Sickle Cell Trait).Watu wenye aina hii ya sickle cell huwa na afya nzuri ya kawaida.

Ugonjwa wa sickle cell ni ugonjwa sugu na wa kudumu.Waathirika waweza kuwa wenye afya njema lakini maisha yao huandamwa na vipindi vya mashambulizi ya maumivu.Umri wa kuishi hupungua na baadhi ya tafiti za nyuma zinaonyesha kwamba waweza kuishi kwa wastani wa miaka arobaini (40) mpaka hamsini (50).Ugonjwa huu ni wa kawaida kwa watu wenye asili ya kiafrika haswa walioko chini ya Jangwa la Sahara lakini waweza athiri watu wa mataifa mengine pia.

Jinsi ugonjwa unavyorithiwa

Ugonjwa wa sickle cell waweza kurithiwa kama ilivyo kwa makundi ya damu, rangi ya ngozi, rangi ya macho na tabia ua vitu vingione vinavyoweza kurithiwa.

Kwa mfano kama mzazi mmoja ana himoglobini AS,amabyo huashiria kuwepo kwa sickle cell bila kuonyesha dalili na mzazi akiwa mzima, basi wana uwezekano wa kupata watoto wenye sickle cell ambao hawataonyesha dalili.

Pia kama mzazi mmoja ana sickle cell na mwingine ana sickle cell bila dalili, kuna uwezekano wa asilimia hamsini ya kupata mtoto mwenye sickle cell au sickle cell bila dalili katika kila mimba itakayotungwa.

Na kuna takriban asilimia ishirini na tano ya kupata sickle cell yenye dalili katika kila mimba.

Jinsi Sickle Cell inavyotokea
Ugonjwa wa sickle cell hutokea kutokana na mabadiliko (mutations) katika mnyororo wa beta (beta chain) ambapo amaino asidi (amino acid) aina ya glutameti (glutamate) huitoa amaino asidi ya Valini (Valine) kutoka kwenye nafasi ya sita ya mnyororo wa beta.

Katika mazingira yenye kiwango kidogo cha oksijeni, chembe hai nyekundu za damu zenye umbo la kawaida (mviringo) huharibiwa na kupoteza uwezo wa kutanuka na kusinyaa (elasticity) zipitapo kwenye mishipa ya damu.Hali hii hupelekea chembe hai hizo nyekundu za damu kuharibiwa na mfumo wa damu kwenye bandama (spleen) uitwao kwa kitaalamu reticuloendothelial system.

Pia hupelekea kuziba kwa mishipa midogo ya damu (infarction) kutokana na chembe hai nyekundu za damu zenye umbo la mundu.Hali hii yaweza kupelekea kukosekana kwa damu na oksijeni ya kutosha katika baadhi ya viungo.

Dalili za sickle cell

Ni mara chache kwa dallili za sickle cell kuonekana katika miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa.Hii inatokana na kuwepo kwa wingi kwa himoglobini ya kichanga, himoglobini F, ambayo huzilinda chembe hai nyekundu za damu zisibadilike umbo.
Ikumbukwe kwambamabadiliko ya kiumbo ya chembe hai nyekundu za damu ndiyo chanzo cha dalili tutakazoziona hivi punde.

Dalili utotoni
-Maumivu ya pingili (dactylitis) za mikono na miguu
-Kushambuliwa na maradhi kama uti wa mgongo,
nimonia,mafua,kikohozi n.k
-Kuvimba kwa bandam (splenomegally) kutokana na kujaa ghafla
kwa damukwenye bandama
-Kusinyaa kwa bandama(autosplenectomy)

Dalili ukubwani

-Upungufu wa damu
-Maumivu ya tumbo
-Maumivu ya mifupa (viungo)
-Kupooza
-Maumivu ya kifua yafananayo na nimonia (acute chest syndrome)
-Kubana kwa kifua
-Kukojoa damu
-Vidonda sugu miguuni
-Kusimaama kwa uume kuambatanako na maumivu makali (priapism)
-Kuvimba kwa paji la uso au fuvu

Vipimo na Uchunguzi

Vipimo vifuatavyo ni muhimu katika kugundua sickle cell na magonjwa yaambatanayo na sickle cell
-Kipimo cha Sickling (Sickling Test)
-Kipimo cha damu kama kuna Malaria
-Kipimo cha mkojo kuchunguza uwepo wa chembe hai nyekendu za damu katika mkojo
-Picha ya kifua (x-ray) kuangalia iwapo kuna athari katika kifua
-Kipimo cha wingi wa damu (Hb level)
-Kipimo cha kundi la damu (Blood grouping and cross matching)

Matibabu

Aina ya matibabu anayohitaji mgonjwa hutegemeana na aina ya mgonjwa na tatizo linalomsumbua kwa wakati huo. Ni vyema kuchukua hatua mapema iwapo una mtoto mwenye dalili zilizotajwa hapo juu.

Ushauri

Ugonjwa wa Sickle cell ni ugonjwa sugu na wa kudumu.Watu wenye ugonjwa huu huambukizwa kirahisi magonjwa mengine kama vile nimonia, malaria n.k

Wagonjwa wenyewe wanatakiwa kujilinda dhidi ya baridi, magonjwa ya kuambukiza kama nimonia, malaria, magonjwa ya mifupa n.k

Pia ni vizuri kwa mgonjwa wa nimonia kuoa au kuolewa na mwenza ambaye hana sickle cell ili kupunguza uwezekano wa kupata mtoto mwenye sickle cell.

Kwa wakina mama wenye sickle cell na wenye mpango wa kubeba ujauzito ni vema wakafahamu kwamba upo uwezekano wa mtoto kudumaa kiakili akiwa tumboni, kutoka ghafla kwa mimba na kupata kifafa cha mimba. Pia ni vizuri kwa wagonjwa wa aina hii kutiwa moyo
.


____________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 25 Novemba 2007)____________________________________________________________
Ukweli Kuhusu Vidonda Vya Tumbo
(Peptic Ulcers
)

Karibuni tena wapenzi wasomaji katika safu hii ya Daktari wako na leo nitapenda kuzungumzia kuhusu ugonjwa wa vidonda vya tumbo ambao kwa kitaalamu hujulikana kama Peptic Ulcer Disease.

Utangulizi

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni ugonjwa ambao unatokana na kumomonyoka (erosion) au kutoboka kwa tabaka la juu la utumbo.

Kwa kawaida tabaka la juu la utumbo hulindwa na ukingo maalum (gastric mucosal barrier) kwa kutengeneza ute (mucous) na alkali za madini ya baikaboneti (bicarbonate ions) dhidi ya tindikali na kimeng’enya (enzyme) cha pepsini.

Mgawanyiko na utengenezwaji wa seli mpya za tabaka la juu la utumbo pamoja na uwepo wa damu ya kutosha ni baadhi ya vigezo vingine vinavyosaidia kulinda tabaka hili na utumbo dhidi ya kumomonyoka au kutoboka.

Kuwepo kwa kigezo chochote kitakachoingiliana na ulinzi dhidi ya tabaka la juu la utumbo hupelekea kumomonyoka kwa tabaka hilo na kusababisha kidonda au vidonda vya tumbo ambavyo huweza kupelekea hata kutoboka kwa utumbo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Aina za Vidonda vya Tumbo

Kuna aina kuu mbili za vidonda vya tumbo.Aina ya kwanza ni ile inayoathiri tumbo (gastric ulcers) na aina ya pili ni ile inayoathiri utumbo mwembamba wa duodeni (duodenum) ambayo kwa kitaalamu hujulikana kama duodenal ulcers.Aina zote mbili kwa ujumla huitwa peptic ulcers.

Hapo zamani ilikuwepo dhana kwamba msongo wa mawazo (stress) na mlo (diet) husababisha vidonda vya tumbo.Baadaye watafiti wa masuala ya afya ya binadamu waligundua akuwa tindikali izalishwayo tumboni na vimeng’enya vya pepsini vinachangia katika kusababisha vidonda vya tumbo.

Hivi karibuni utafiti umeonyesha kwamba zaidi ya asilimia themanini ya vidonda vya tumbo hutokana na bakteria aitwaye Heliocobacter pylori (H.pylori).Ingawa inasadikika kwamba vigezo vyote hapo juu huchangia kupata vidonda vya tumbo,bakteria H.pylori anasadikiwa kuwa chanzo kikuu katika kusababisha vidonda vya tumbo.

Vidonda vya tumbo (gastric ulcers) na dalili zake

Asilimia kubwa ya waathirika wa aina hii ya vidonda vya tumbo ni watu wenye umri zaidi ya miaka arobaini (40) na wanaume huathirika zaidi kuliko wanawake.Waathirika wa aina hii ya vidonda vya tumbo huwa wembamba kutokana na kutokula wakihofia kupata maumivu pindi walapo chochote.Dalili kubwa ya wagonjwa hawa ni maumivu ya tumbo (chembe).Maumivu yake huwa yenye majira maalum ambapo huanza punde tu mgonjwa alapo chakula na hupungua baada ya chakula kuisha tumboni au kwa kunywa kimiminika chenye alkali.Hamu ya kula huwa nzuri lakini baadhi yao waweza kutapika.Kutapika damu (haematemesis) na kupata choo chenye damu (malaena) huweza kuambatana na aina hii ya vidonda vya tumbo.Uzito wa mwili hupungua kwa kiasi fulani kutokana na kutokula vizuri.Kusambaa kwa maumivu mpaka mgongoni kwaweza kutokea iwapo kidonda kimetoboka na kuhusisha kongosho (pancreas).

Vidonda vya Utumbo mwembamba (duodenal ulcers) na dalili zake

Aina hii ya pili kwa upande mwingine huathiri watu wenye umri chini ya miaka arobaini (40) na kama aina ya kwanza,waathirika wengi ni wanaume.Maumivu, tofauti na aina ya kwanza, hutokea kati ya masaa mawili na nusu hadi manne bada yamlo ambapo chaklula huwa kimeisha tumboni (hunger pains).Maumivu pia hutokea zaidi mapema asubuhi au nyakati za jioni.Nafuu hupatikana kwa kula chakula.

Kutapika hutokea kwa nadra sana kwa wagonjwa wa aina hii.Hata hivyo kutapika damu na kupata choo chenye damu hutokea mara nyingi zaidi kuliko aina ya kwanza.Hamu ya kula kwa wagonjwa wa aina hii huwa nzuri na hupenda kula mara kwa mara hivyo huwa na miili yenye afya nzuri tofauti na wagonjwa wa aina ya kwanza.

Jinsi H.pylori anavyosababisha vidonda vya tumbo
Kuathirika na vimelea vya H.pylori ni kawaida kwa mwanadamu yeyote.Takwimu za Uingereza zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia hamsini ya idadi ya watu wazima wameathirika na bakteria hao.Idadi ni kubwa, zaidi ya asilimia tisini, kwa baadhi ya nchi nyingine.

Hata hivyo ni baadhi tu ya watu kati ya walioathirika na vimelea vya bakteria hawa hupata vidonda vya tumbo.Hakuna sababu za kisayansi zinazoelezea hali hiyo.

Vimelea vya H.pylori huweza kusambaa kupitia chakula na maji.Vimelea vya bakteria hawa pia hupatikana kwenye mate hivyo vyaweza kuambukizwa kupitia kinywa haswa iwapo mtu atabusiana na muathirika wa vimelea hivyo.Watu wengi pia huathirika na vimelea hivi utotoni.

Vimelea vya H.pylori huweza kuishi kwenye ute ulindao tabaka la juu la tumbo na utumbo mpana.Hapo hutengeneza kimeng’enya kiitwacho urease ambacho hupunguza makali ya tindikali izalishwayo na tumbo.Ili kukabiliana na hali hii,tumbo hutengeneza tindikali nyingi zaidi ambayo huathiri tabaka la juu la utumbo.Vimelea hivi pia hudhoofisha ute ulindao tabaka la juu la utmbo hivyo kushindwa kulinda tumbo na utumbo mwembamba sawasawa.

Aidha,vimelea vya H.pylori hujiegesha kwenye seli za tumbo.Hali hii hudhoofisha mfumo wa ulinzi wa tumbo na kusababisha maumivu na hatimaye madhara katika eneo lililoathirika.

Vigezo hatarishi

Vifuatavyo ni vigezo hatarishi ambavyo vyaweza kuongeza uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.

Madawa ya Kupunguza Maumivu
Dawa hizi ambazo hujulikana pia kama Non Steroidal Anti Inflammatory Drrugs (NSAIDs) hupunguza uwezo wa tumbo kutengeneza ute ulindao utumbo hivyo kuongeza uwezekano wa tabaka la juu la utumbo kumomonyolewa na tindikali.Madawa haya pia yaweza kuathiri upatikanaji wa damu ya kutosha tumboni na uwezo wa mwili haswa utumbo kutengeneza seli mpya.Dawa hizi ambazo hutumika kutibu maumivu ya kichwa na misuli ni Aspirin, Ibuprofen n.k

Sababu za kijenetiki
Historia ya kuwepo kwa kwa vidonda vya tumbo katika ukoo au familia yaweza kuchangia ndugu wa ukoo au familia husika kupata vidonda vya tumbo.Pia, tafiti zimeonyesha uhusiano kati ya watu wenye kundi la damu la O (blood group O) na uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.

Uvutaji wa sigara
Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuongezeka kwa uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo kutokana na kuvuta sigara.Uvutaji wa sigara huchelewesha kupona kwa kidonda na huchangia kutokea tena kwa kidonda.

Unywaji pombe
Kama ilivyo sigara, pombe huathiri tabaka la utumbo na kupunguza utengenezwaji wa ute ulindao tabaka hilo.

Kafeini (Caffeine)
Kafeini ambayo hupatikana kwenye baadhi ya vinywaji kama soda, kahawa n.k huchangamsha utengenezaji wa tindikali tumboni ambayo hutonesha kidionda kilichopo.

Msongo wa Mawazo
Msongo wa mawazo hausababishi vidonda vya tumbo badala yake huongeza maumivu kwenye kidonda kilichopo.Hufanya hivyo kwa kuongeza zaidi utengenezwaji wa tindikali tumboni.

Uchunguzi na Matibabu
Uchunguzi hujikita zaidi kwenye kuona iwapo utumbo umeathirika na kidonda (vidonda) na pia kwa kuthibitisha uwepo wa vimelea vya bakteria wa H.pylori.
Uchunguzi iwapo utumbo umeathirika na vidonda (endoscopy) hufanywa kwa kutumia tyubu maalum iingizwayo kwenye njia ya chakula hadi kwenye utumbo mwembamba.Kipande cha nyama (biopsy) ya tabaka la juu la utumbo chaweza kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi kwenye hadubini iwapo kuna vimelea vya H.pylori au saratani.
Baadhi ya majaribio maalum kugundua uwepo wa vimelea vya H.pylori ni pamoja na kipiomo cha damu (serology), kipimo cha kupumua urea (urea breath test), kipimo cha kugundua kingamwili kwenye choo (stool antigen test) n.k

Matibabu hujumuisha dozi ya dawa tatu za mseto.Mbili za kiuavijasumu (antibiotic) na moja dhidi ya tindikali (proton pump inhibitor) kwa muda wa juma moja au zaidi.

Ushauri
Ni vyema kumuona daktari ili ufanyiwe uchunguzi na kupatiwa tiba sahihi iwapo una dalili zilizotajwa hapo juu.
Pia ni muhimu kuzingatia dozi kwa kunywa dawa katika muda uliopangwa na kumaliza dozi hata baada ya dalili (maumivu) kupotea.

Ugonjwa wa vidonda vya tumbo tofauti na inavyodhaniwa waweza kupona kabisa kama magonjwa mengine.
Madhara kama kutoboka kwa utumbo,kuvuja damu, kuziba kwa tumbo na saratani ya tumbo yanaweza kutokea iwapo tiba haitatolewa katika muda muafaka.

_____________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 4 Novemba 2007)

_______________________________________________
Magonjwa Nyemelezi na dalili zake

Wapendwa wasomaji wiki hii nitapenda kuzungumzia juu ya magonjwa nyemelezi. Magonjwa nyemelezi si neno geni miongoni mwa watu wengi haswa katika miongo hii miwili toka kugundulika kwa ugonjwa wa Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) na Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Utangulizi

Magonjwa nyemelezi ni yale ambayo hushambulia mwili wa binadamu pale uwezo wa kinga ya mwili kupigana na vimelea vya magonjwa unaposhuka.Ni magonjwa ambayo katika hali ya kawaida hayategemewi kujitokeza kwa mtu mwenye kinga kamili ya mwili.
Kwa kawaida mwili wa binadamu yeyote umeumbwa na kinga ya mwili ya asili ambayo lengo lake kuu ni kuulinda mwili dhidi ya vimelea vya magonjwa.Inapotokea kimelea (vimelea) kuingia katika mwili wa binadamu kwa njia yoyote (kunywa au kula vimelea,kugusana na majimaji au ngozi ya mtu mwenye vimelea,au kupitia damu yenye vimelea n.k), mwili hutengeneza kingamwili (antibodies) ambazo hupigana na vimelea hivyo ili kuuweka mwili katika afya njema kama hapo awali.

Kushuka kwa kinga ya mwili hupelekea mwili kushindwa kupigana na vimelea vya magonjwa hivyo kusababisha kushambuliwa na magonjwa.Ifahamike kwamba baadhi ya vijidudu(microorganisms) pia hupatikana katika mwili wa binadamu bila madhara yoyote (normal flora) kama vile kwenye ngozi, mfumo wa chakula, ukeni, uumeni n.k Hata hivyo vijidudu hivi huweza kuwa chanzo cha magonjwa iwapo kinga ya mwili itashuka.
`
Vitu gani hupelekea kushuka kwa kinga ya mwili?

Sababu mojawapo kubwa ya kushuka kwa kinga ya mwili haswa katika nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara ni Ukimwi/VVU.Hata hivyo ieleweke kwmba si kila mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini ana VVU.

Kuna sababu nyingine nyingi ambazo husababisha kwa njia moja au nyingine kushuka kwa kinga ya mwili.Zifuatazo ni baadhi tu ya sababu hizo;

Utapiamlo, Kuugua mara kwa mara,Sababu za kijenetiki (kurithi),Madhara kwenye ngozi,Msongo wa mawazo na Ujauzito. Madawa ya Kutibu saratani, Matumizi ya muda mrefu ya antibayotiki (antibiotics),steroidi (steroids) na madawa ya kushusha kinga mwilini (immunosuppressant drugs)) ambayo hutumika wakati wa kupandikiza viungo mwilini kama figo n.k

Magonjwa nyemelezi husababishwa na vijidudu mbalimbali kama bacteria,virusi,fangasi na bakteria.

Bakteria
Baadhi ya magonjwa yasababishwayo na bakteria ni kama yafuatayo;

Kifua Kikuu (TB)
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea kiitwacho Mycobacterium tuberculosis ambacho ni moja katika kundi la Mycobacterium Avium Complex (MAC).Kushuka kwa kinga ya mwili hupelekea kulipuka kwa vimelea vya kifua kikuu ambavyo hupatikana, pamoja na viungo vingine, zaidi kwenye mapafu.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kikohozi na homa (haswa nyakati za usiku) kwa zaidi ya wiki mbili.Kutokwa jasho usiku (mara nyingi jasho huwa jingi mpaka kulowesha shuka),kupungua uzito (zaidi ya kilo moja na nusu ndani ya mwezi), Kichomi na kukohoa damu.
Ugonjwa huu pia huweza kupelekea kupata homa ya uti wa mgongo(meningitis) ambayo huambata na dalili kama kuumwa kichwa, kichefu chefu na kutapika ikifutiwa na kuongezeka kwa joto la mwili na maumivu na kukaza kwa shingo.




Nimonia (Pneumonia)
Huu ni ugonjwa ambao kwa kiasi kikubwa huathiri mfumo wa hewa na haswa mapafu.Baadhi ya vimelea viletavyo nimonia ni kama Pneumococcus ,Haemopilus influenza, Mycoplasma (haswa kwa watoto) pia Klebsiella, Staphylococcus aureus, Pseudomonas aeuroginosa (kwa wagonjwa waliolazwa mahospitalini) na wengineo.
Ugonjwa huu huanza ghafla na dalili zake ni kama homa kali, kikohozi, maumivu wakati wa kupumua, baridi na kutetemeka.

Ugonjwa wa Ngozi
Huu husababishwa na vimelea vya Staphylococcus aureus.Vimelea hivi huishi katika mwili wa binadamu (kwenye ngozi ya kichwa na kinena (groins) na kwapani) bila madhara.Pia hupatikana kooni na katika utumbo mpana na mkojo.
Vimelea vya Staphylococcus husambaa kwenda sehemu nyingine ya mwili kutoka kwenye usaha, mgusano na ngozi ya mwenye maradhi, kutumia taulo, matandiko,vifaa vya mtu aliyeathirika n.k

Dalili zake ni pamoja na chunusi, majipu, kubabuka kwa ngozi na magamba magamba katika ngozi.


Magonjwa ya Virusi

Magonjwa yasababishwayo na virusi ni kama;

Ugonjwa wa Malengelenge
Husababishwa na virusi vya Herpes Simplex.Hivi vimegawanyika katika Herpes Simplex Virus-1 (HSV-1) na Herpes Simplex-2 (HSV-2).Virusi vya HSV-1 vyaweza ambukizwa kupitia ngozi laini (mucous membranes) za mwili na kubusiana.Huweza kusababisha mwasho kwenye midomo,ulimi,fizi za meno au kingo za juu za kinywa (buccal mucosa).Kwa upande wa virusi vya HSV-2 hivi huweza kusababisha michubuko na maumivu kwenye uume,uke na njia ya haja kubwa.

Katika kiwango cha juu cha ugonjwa viungo vingine vya mwili kama macho, njia ya chakula, mfumo wa fahamu na na njia za mfumo wa hewa huathirika.

Dalli balimbali za ugonjwa huu ni malengelenge (blisters), mwasho na muunguzo.Kushindwa kumeza au kupata maumivu wakati wa kumeza (haswa chakula),tezi kuvimba na maumivu wakati wa haja kubwa au ndogo.

Mkanda wa jeshi
Husababishwa na kirusi kiitwacho Varicella Zoster (VSV).Mara nyingi hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa ambao ulikuwepo mwilini hapo Awali (reactivation of an earlier infection).Mbali ya kuathiri ‘uwanda’ (dermatome) moja au zaidi wa mishipa ya fahamu (neva),pia huweza kudhuru jicho (herpes zoster opthalmicus) na sikio (herpes zoster oticus).
Dalili zake ni maumivu makali katika ‘uwanda’ ulioathirika, homa, vipele, maumivu ya kichwa, uchovu na maumivu ya macho kutokana na mwanga (photophobia).

Maumivu ya Retina
Kwa lugha ya kitaalamu huitwa CMV Retinitis na husababishwa na kirusi kiitwacho Cytomegalovirus (CMV).Kirusi hiki, mbali ya kuathiri jicho na haswa retina, pia huathiri viungo vingine kama mapafu na kusababisha nimonia, utumbo mpana na mfumo wa fahamu ambako husababisha maumivu.

Dalili zake ni pamoja na kutoona vizuri, macho kuuma, kutokwa na machozi kwa wingi.Kutopata matibabu mapema huweza kusababisha upofu.Pia Huweza kuathiri viungo vingine na kusababiosha homa, nimonia, kichefuchefu, kuharisha na kupungua uzito.

Magonjwa yatokanayo na Fangasi

Fangasi pia huweza kujitokeza iwapo kinga ya mwili itashuka.



Kandidiasisi
Ugonjwa huu uliozoeleka pia hujulikana kwa kitaalamu kama Candidiasis.Kandidiasisi husababishwa na fangasi aitwaye Candida albicans ambaye huathiri kinywa, mfumo wa chakula,uke na mfumo wa hewa.Kandidiasisi katika uke huweza tokea kwa mwanamke mwenye afya asiye na VVU.

Dalili za Kandidiasisi katika kinywa ni pamoja na kubadilika kwa ladha,maumivu kwenye ulimi,utando mweupe kwenye ulimi na kingo za juu za kinywa (buccal mucosa),kushindwa kumeza,maumivu wakati wa kumeza chakula ikiwa fangasi imesambaa sana. Pia mwasho na maumivu ukeni pamoja na kutokwa na majimaji meupe ukeni.

Homa ya Uti wa mgongo
Homa ya utiw amgongo au Meningitis kwa kitaalamu husababishwa na fangasi aitwaye Cryptococcal neoformans.Uti wa mgongo utokanao na aina hii ya fangasi huweza kusababisha kifo usipotibiwa.Aina hii ya fangasi ambayo huathiri zaidi ubongo na uti wa mgongo, hutokana na kuvuta hewa yenye vumbi litokanalo na ndege lenye vimelea vya ugonjwa.
Baadhi ya dalili zake ni homa, kutoona vizuri,macho kuuma kutokana na mwanga,kuchanganyikiwa akili,maumivu ya kichwa ka kukakamaa na kuuma kwa shingo.

Histoplasmosisi
Aina hi ya fangasi hutokana na vimelea vya Histoplasma capsulatum.Fangasi huyu huathiri mapafu pamoja na viungo vingine.Dalili zake ni homa,uchovu,kupungua uzito na kupumua kwa shida.Pia kukohoa na kuvimba kwa tezi kwaweza kutokea.


Nimonia
Kama bakteria na fangasi pia huweza kusababisha nimonia ijulikanayo kwa kitaalamu kama Pneoumocystis Pneumonia (PCP).Vimelea vya Pneumocystis jiroveci (awali vilijulikana kama Pneuomocystis carinii) huathiri mfumo wa hewa.Fangasi huyu pia huweza kuathiri viungo vingine kama ini,wengu (spleen) na figo katika baadhi ya wagonjwa.
Dalili zake ni kikohozi kikavu,kifua kubana,kupumua kwa shida,homa,kuishiwa pumzi na kutokwa jasho nyakati za usiku.

Magonjwa yatokanayo na Protozoa

Toksoplasmosisi ya Ubongo
Cerebral toxoplasmosis, kama ujulikanavyo kitaalamu,hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa wa awali kutokana na vimelea vya Toxoplasma gondii (kimelea kiwezacho kuishi ndani ya seli kinachoathiri ndege,wanyama na binadamu).Kimelea hiki kiathiricho zaidi mfumo wa fahamu,hupatikana kwenye nyama isiyopikwa vizuri na mavi ya paka.Huathiri zaidi ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa,kuchanganyikiwa,udhaifu wa viungo,homa,kupoteza fahamu,kupooza na kifafa.

Kriptosporidiosisi
Huu ni ugonjwa utokanao na vimelea vya Cryptosporidium.Huathiri zaidi mfumo wa chakula na hutokana na kutumia kwa maji au chakula vilivyoathirika na vimelea vya ugonjwa huu.Dalili zake ni kuharisha sana kiasi cha kusababisha kupungukiwa na maji mwilini (dehydration),maumivu wakati wa haja kubwa, kichefuchefu na kutapika.Wagonjwa wa aina hii huwa na joto la mwili la kawaida.

Matibabu na Ushauri

Aina ya matibabu hutegemea na aina ya ugonjwa na mtu, pia kutokana na kuwepo kwa Ukimwi/VVU hutegemea kiwango cha seli za CD4 mwilini.Iwapo una dalili kati ya zilizotajwa hapo juu ni vyema kumona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Ni vyema kuzingatia kuwepo kwa dalili zilizotajwa hapo juu hakumanishi kuwa muathirika ana VVU na si kila mwenye VVU huwa na dalili hizo.Pia kujitokeza kwa dalili kunaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.Hata hivyo ni vyema kupima afya yako kila mara haswa VVU ili kujua chanzo cha kupungua kwa Kinga ya mwili ambayo huweza kupelekea kupata magonjwa nyemelezi

_________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 4 Novemba 2007)
_________________________________________
Ugonjwa wa Kisukari na athari zake

Juma lililopita nilizungumzia ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na athari zake.Jumapili ya leo nitapenda tuangalie ugonjwa mwingine sugu wa kisukari ama kwa lugha ya kitaalam Diabetes mellitus.

Utangulizi

Ugonjwa wa kisukari au Kisukari kama kilivyozoeleka miongoni mwetu, ni ugonjwa utokanao na kiwango kikubwa cha sukari katika damu. Sukari katika damu hutokana na kumeng’enywa kwa wanga (carbohydrate).

Kwa kawaida sukari katika damu hukupa nishati ambayo hukuwezesha kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli, kufanya mazoezi na kufanya shughuli zako za kila siku.Insulini ni homoni ibadilishayo sukari iliyoko kwenye damu kuwa nishati.Homoni hii hutengenezwa na aina ya seli ziitwazo beta (beta cells) ambazo hupatikana kwenye kongosho (pancreas).Insulini ni moja kati ya homoni zihusikazo na usimamizi wa kiwango cha sukari katika damu.Kwa mfano, endapo kiwango cha sukari katika damu kitapanda, insulini hufanya kazi ya kukipunguza kufikia kiwango cha kawaida kitakiwacho kwenye mwili wa binadamu mwenye afya njema.Hufanya hivyo kwa kuruhusu sukari iliyopo kwenye damu kuingia kwenye ini, misuli na seli za mafuta (fat cells) ambako hutumika kama nishati.

Mtu mwenye kisukari ni yule ambaye ama mwili wake umeshindwa kutengeneza insulini au kiwango cha insulini ni kidogo kuliko mahitaji yake au mwili umeshindwa kutumia insulini iliyopo.

Kwa nini watu hupata kisukari?

Awali ya yote ni vema ukafahamu kwamba kuna aina mbili kuu za kisukari.Aina ya kwanza ni ile ya kisukari kitegemeacho insulini (Insulin Dependent Diabetes Mellitus) na nyingine ni kisukari kisichotegemea insulini (Non Insulin Dependent Diabetes Mellitus). Baadhi ya vyanzo hujumuisha Kisukari kitokanacho na Ujauzito (Gestational Diabetes) kama aina ya tatu ya kisukari.

(i) Kisukari Kitegemeacho Insulini

Katika aina hii ya kisukari mwili wa binadamu hushindwa ama kutengeneza homoni ya insulini au hutengeneza insulini kidogo sana ambayo hushindwa kusimamia kiwango cha sukari kwenye damu. Kutokana na takwimu za nchini Marekani, aina hii ya kisukari inasemekana kuathiri karibu asilimia kumi (10%) ya wagonjwa wote wa kisukari. Aina hii ambayo kwa kawaida hugundulika utotoni au ujanani, pia yaweza kumtokea mtu mzima endapo kongosho yake imeharibika kutokana na pombe, ugonjwa au kuondolewa kutokana na upasuaji.Watu wenye aina hii ya kisukari kwa ujumla huhitaji matibabu ya kila siku ya insulini ili waendelee kuishi.

Sababu za mtu kupata aina hii ya kisukari ni kama zifuatazo:

Mosi ni sababu za kijenetiki.Hizi huchangia karibu theluthi moja ya uwezekano wa kupata kisukari kitegemeacho insulini.Tafiti mbalimbali zinazohusiana na seli za binadamu zimeonyesha uhusiano mkubwa kati ya aina hii ya kisukari na antijeni za chembe hai nyeupe za binadamu (Human Leucocyte Antigen-HLA) haswa zile za aina ya HLA-DR3 na HLA-DR4 kwa karibu ya asilimia 95 ya wagonjwa.

Sababu ya pili inayohusishwa na aina hii ya kisukari ni iwapo mgonjwa wa kisukari alishawahi kuugua ugonjwa utokanao na virusi.Uthibitisho unapatikana kutokana na tafiti zilizofanywa na ambapo chembechembe za virusi zimegundulika kusababisha madhara dhidi ya kinga ya mwili (autoimmune damage) kwa seli zihusianazo na kinga kudhuru seli zake zenyewe hasa zile za beta zilizopatikana toka kwenye kongosho. Baadhi ya virusi vihusishwavyo ni Rubella, Epstein Barr, Cytomegalovirus, Coxsackie B4 na Mumps; ingawa jinsi virusi hivyo vinavyodhuru bado haijafahamika.

Aina ya mlo ni sababu ya tatu iletayo kisukari kinachotegemea insulini. Aina ya protini ipatikanayo kwenye damu ya ng’ombe na ambayo ni sehemu kubwa inayotengeneza maziwa ya ng’ombe imeonekana kuchokoza uwezekano wa kupata aina hii ya kisukari. Imegundulika kwamba watoto walionyweshwa maziwa ya ng’ombe mapema utotoni wana asilimia kubwa ya kupata aina hii ya kisukari kuliko wale walionyonyeshawa titi la mama.

Msongo wa mawazo pia waweza changia kupata kisukari kinachotegema insulini kwa kuchochea mwili kutengeneza homoni zipinganazo na hali ya msongo wa mawazo.

Aina hii ya kisukari huwa na sifa zifuatazo:
Huanza kabla ya mtu kufikisha umri wa miaka arobaini, umbile la mwili huwa la kawaida au hupungua (kukonda), kiwango cha insulini kwenye damu huwa chini wakati kiwango cha glukagoni (homoni ibadilishayo glaikojeni kuwa sukari) huwa juu.

Dalili zake huonekana mapema kama kuwa na kiu sana, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito mbali ya kula sana, kuchoka choka, kichafuchefu na kutapika.

(ii) Kisukari kinachotegemea insulini

Aina hii ya pili ya kisukari hutokea sana kwa watu wanene kupita kiasi.
Katika aina hii mwili hutumia kidogo au kushindwa kabisa kutumia insulini iliyotengenezwa na kongosho. Kutoitambua insulini kufanywako na seli za mwili (insulin resistance) husababisha mwili kutengeneza insulini nyingi zaidi.Takriban asilimia tisini ya wagonjwa wa kisukari huugua aina hii.

Sabau zihusianazo na aina hii ya Kisukari ni pamoja na sababu za kijenetiki.Jinsi ambavyo sababu za zinachangia hali hii haijulikani lakini jeni (genes) kadhaa zinahusishwa. Hakuna uhusiano na antijeni za chembe hai nyeupe za binadamu.Pia seli za beta, tofauti na kwenye aina ya kwanza, huwa hazijadhurika.

Sababu ya pili ni mwenendo wa maisha.Tabia ya kula kupita kiasi na kuzidi mahitaji ya mwili haswa kwa watu wanene kupita kiasi huchangia katika kupata aina hii ya pili ya kisukari.Unene wa kupita kiasi hufanya insulini kutofanya kazi sawasawa kwa kuongeza ukinzani wa seli katika kuzitambua insulini.

Utapiamlo wa mtoto akiwa tumboni pia umehusishwa na aina hii ya kisukari.Inasemekana kwamba utapiamlo hata ule wa mtoto mchanga aliye chini ya mwaka mmoja huweza kuzidhuru seli za beta zisikue vizuri katika kipindi muhimu cha ukuaji na hivyo kumhatarisha muathirika huyo kupata aina hii ya kisukari baadaye maishani.

Baadhi ya sifa ziambatanazo na aina hii ya kisukari ni pamoja na kuanza baada ya umri wa miaka arobaini, mgonjwa kuwa mnene kupita kiasi, kiwango cha insulini katika damu kuwa kawaida au juu na kiwango cha homoni ya glukagoni kuwa kuwa juu.Pia dalili za ugonjwa huchukua kati ya miezi hadi miaka kuonekana.Dalili hizo ni kuwa na kiu sana, kukojoa mara kwa mara, kuongezeka kwa hamu ya kula, kuchokachoka, kutoona vizuri, mgonjwa kuchelewa kupona baadhi ya magonjwa hasa vidonda na kupungua kwa nguvu za kiume.

(iii) Kisukari kitokanacho na Ujauzito

Aina hii ya kisukari hutokea zaidi kati ya nusu ya pili ya ujauzito yaani kati ya miezi minne na nusu hadi miezi tisa.Ingawa aina hii ya kisukari huisha baada ya kujifungua, wanawake wenye aina hii ya kisukari wana nafasi kubwa kuliko wanawake wengine, ya kupata kisukari kisichotegemea insulini baadaye maishani.

Vigezo hatarishi kwa mtu kupata kisukari:

Kuwa na ndugu (mzazi, kaka au dada) mwenye kisukari

Unene wa kupita kiasi

Umri wa zaidi ya miaka arbaini na mitano (45)

Kuwa shinikizo la juu la damu

Kuwa na kiwango kikubwa cha mafuta (triglycerides) kwenye damu

Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) kwenye damu

Kutokufanya mazoezi ya kutosha

Dalili za jumla za ugonjwa wa kisukari ni kama zifuatazo:

Dalili ya kwanza ni Uchovu.Kwa mtu mwenye kisukari, mwili hushindwa au hutumia kwa kiasi kidogo sukari kama nishati mwilini na badala yake hutumia mafuta yaliyoko mwilini.Mchakato huu huugharimu mwili kutumia nishati zaidi na matokeo yake mtu hujisikia mchovu.

Dalili ya pili ni kupungua uzito pasipo sababu.Mtu mwenye kisukari hushindwa kutumia chakula anchokula kutengeneza nishati kwahiyo anaweza kupungua uzito mbali ya kuwa anakula vizuri.Kitendo cha kupoteza sukari na maji kwenye mkojo pamoja na kupungukiwa maji mwilini pia huchangia kupunguza uzito.

Dalili nyingine ni kunywa maji mengi.Mgonjwa wa kisukari huwa na sukari nyingi kwenye damu.Mwili hujaribu kupambana na hali hii kwa kutuma ujumbe kwenye ubongo kupunguza usukari kwa kunywa maji mengi ili pia kulipizia kiasi kilichopotea kutokana na kukojoa sana.

Kukojoa sana ni dalili nyingine ambapo mwili hutumia njia hii katika kujaribu kupunguza kiwango cha ziada cha sukari kwenye damu kupitia kwenye mkojo.

Dalili ya tano ni kula sana.Hali hii hutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha insulini katika mwili.Wingi wa insulini mwilini ni matokeo ya kongosho kuzalisha insulini ili kukabiliana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu.Pia kutokana na seli za mwili kutotaimbua insulini kama tulivyoona kwenye kisukari kisichotegemea insulini,homoni hii huwa nyingi mwilini.

Kuchelewa kupona kwa kidonda ni dalili mojawapo ya kuwepo kwa ugonjwa wa kisukari mwilini.Sukari nyingi katika damu huzuia chembehai nyeupe za damu kutokufanya kazi sawa sawa ya kulinda mwili dhidi ya bakteria na kuondoa seli zilizokufa toka mwilini.

Magonjwa katika njia ya mkojo (urinary tract infection), kwenye sehemu za siri (haswa ya fangasi), kushuka kwa kinga ya mwili kutokana na kisukari pamoja na uwepo wa sukari kwenye viungo ambavyo huchochea bacteria kukua vizuri.

Kutoona vizuri pia huweza kuhusiana na kiwango kikubwa cha sukari katika damu ingawa si lazima kuwepo kwake humaanisha kuwepo kwa ugonjwa wa kisukari.

Jinsi ya kudhibiti Kisukari

Kula mlo kamili mara kwa mara.Usikae na njaa.Mlo uwe na mbogamboga za majani zaidi, mafuta kidogo na upunguzwe vitu vitamu kama pipi, keki,chokoleti n.k

Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kupunguza madhara zaidi yatokanayo na kisukari kama magonjwa ya moyo, kiharusi (stroke), upofu na vidonda miguuni.

Punguza au acha kabisa kutumia kileo (pombe).Unywaji wa pombe wa kupindukia ni kigezo hatarishi cha kupata kisukari kisichotegemea insulini.

Acha kuvuta sigara (tumbaku) kwani uvutaji huathiri mishipa ya damu na hupelekea kupata magonjwa ya moyo, kiharusi na huhitilafiana na mzunguko wa damu kwenye miguu.

Dhibiti kiwango chako cha sukari kwenye damu kwa kupima mara kwa mara haswa kabla ya mlo na wakati wa kulala. Zingatia matibabu.

Jiunge na kliniki ya watu wenye kisukari iliyo karibu na wewe ili upate elimu na maelezo zaidi kuhusu ugonjwa wa kisukari. Onana na daktari angalau kila baada ya miezi mitatu.


Madhara zaidi yatokanayo na kisukari

Aina zote za kisukari hupelekea kuzidi kwa kiwango cha sukari kwenye damu. Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa muda mrefu huharibu macho, figo, mishipa ya fahamu (neva) na mishipa ya damu.

Macho
Mabadiliko yanayotokea kwenye jicho ambayo ni maalum kwa kisukari ni pamoja na mishipa ya damu ya retina kuziba, kuwa migumu na kuvujia kwa damu.Dalili za mwanzo ni kupungua kwa uwezo wa kuona, maumivu kutokana na mwanga na hatimaye kutokuona kabisa (upofu).

Figo
Kutokana na wingi wa sukari katika damu pia huweza kusababisha madhara katika figo na kupelekea kupotea kwa sukari na protini kwenye mkojo.Pia husababisha kusimama kwa figo kufanya kazi (renal failure).

Mishipa ya fahamu (Neva)

Madhara katika mishipa ya fahamu hutokana na kisukari sugu au kisichotibiwa sawasawa.Mgonjwa hulalamika maumivu na wakati mwingine ganzi miguuni.Pia huvimba miguu,hukosa haja ndogo au/na kubwa, kutotoka jasho haswa mikononi na miguuni na hushindwa kusimamisha uume kwa wanaume.Inakadiriwa kuwa takriban asilimia hamsini ya wanaume wanaougua kisukari wanashindwa kwa kiasi fulani kusimamisha uume.


Mishipa ya damu

Sukari nyingi katika damu huathiri mishipa ya damu na hivyo kupelekea kupungua kwa hisia.Pamoja na kupungua kwa damu ifikayo miguuni husababisha kuumia kirahisi kwa dole gumba na unyayo ambako hupelekea kidonda. Kidonda cha mguu huweza kupelekea kukatwa kwa mguu.



Kupungua kwa sukari katika damu

Endapo kutakua na insulini nyingi mwilini na sukari kidogo katika damu, huweza kupelekea kushuka chini ya kiwango cha kawaida kwa sukari katika damu.Hali hii pia huweza kusababishwa na kuzidisha kiwango kitakiwacho cha insulini kwa ajili ya matibabu. Dalili ya mwanzo huwa ni njaa, ikifuatiwa na kizunguzungu, kutokwa jasho, moyo kwenda mbio, kuchanganyikiwa na kisha kupoteza fahamu.

Uchunguzi na Matibabu

Kiwango cha sukari katika damu ndicho kigezo pekee cha kugundua iwapo mtu ana kisukari. Sindano huchomwa kwenye kidole na damu huwekwa kwenye utepe maalum (strip) ambao hupitishwa kwenye mashine iwezayo kugundua kiwango cha sukari katiaka damu (random blood glucose).Njia hii huweza kugundua kwa haraka kiwango cha sukari katika damu ingawa si kipimo makini sana.

Vinginevyo mgonjwa hutakiwa kutokula kitu (kufunga) usiku kucha, kwa angalau masaa nane (8) kabla ya kutolewa damu na kupimwa kiwango cha sukari kwenye damu (fasting blood glucose)
Kipimo kingine ambacho sio maalum sana lakini husaidia kuthibitisha uwepo wa kisukari ni kipimo cha mkojo kuchunguza iwapo kuna sukari (glycosuria) au protini (proteinuria).

Matibabu
Kwa kisukari kitegemeacho insulini, tiba yake ni lazima kupata insulini (sindano)kila siku.
Kwa kisukari kisichotegemea insulini, mazoezi, mlo kamili usio na sukari wala mafuta kwa wingi, mazoezi na madawa (haswa ya kumeza) huweza kukidhibiti.

Ni vizuri kumuona daktari iwapo una dalili zilizotajwa hapo juu kwa ushauri zaidi na epuka kutumia dawa bila ushauri wa daktari.
___________________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com, 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 4 Novemba 2007)
____________________________________________________________

Friday, December 21, 2007

Jumamosi Desemba 22,2007.

SHINIKIZO LA JUU LA DAMU (HYPERTENSION)

Wapendwa wasomaji katika makala ya leo ambayo ndiyo ya kwanza katika blogu hii tutatazama Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ambao kwa lugha ya Kitaalamu huitwa “Hypertension” au kwa lugha ya Kigeni “High Blood Pressure”. Ugonjwa huu ni moja ya magonjwa yanayowaathiri watu duniani kutokana na mateso,vifo pamoja na gharama zinazoambatana nao.Ugonjwa huu umekuwa ni moja ya changamoto muhimu katika afya ya jamii
Utangulizi
Kwa kawaida wakati moyo ukisukuma damu katika ateri (mishipa midogo ya damu),damu hiyo hupita kwa nguvu dhidi ya kuta za mishipa hiyo.
Shinikizo la damu hupimwa na kifaa maalum kijulikanacho kitaalum kama sfigmomanometa (sphygmomanometer) na kuweka damu kwa tarakimu mbili kwa mfano 120/80 milimita za mekyuri (zebaki)
Namba ya juu huonyesha shinikizo litakanalo na kutanuka na kusinyaa kwa moyo wakati damu ikisukumwa kutoka katika chemba za moyo kitaalamu huitwa systolic pressure. Namba ya chini yenyewe huonyesha shinikizo katika mishipa ya damu (ateri) wakati damu ikijaa kwenye chemba za moyo kwa kitaalumu huitwa diastolic pressure.
Kipimo cha kawaida cha shinikizo la damu kwa watu wengi ni milimita za mekyuri 120/80 .Chini ya hapo huitwa shinikizo la chini la damu (hypotension) na juu ya kipimo hicho huitwa shinikizo la juu la damu (hypertension) ambalo huanzia milimita za mekyuri 140 kwa “systolic pressure” milimita za mekyuri 90 kwa “diastolic pressure”.
Shinikizo la juu la damu lisilotibiwa linahusishwa na vifo vingi na madhara ya tokanayo na kusimama kwa moyo, kiharusi na figo kushindwa kufanya kazi. Kutokana na tafifi mbalimbali zilizofanywa, hatari ya kufa kutokana na moyo kusimama na inahusishwa moja kwa moja na shinikizo la damu haswa kipimo cha “sistoliki” (systolic). Hata hivyo ongezeko la magonjwa ya moyo kutokana na shinikizo la juu la damu linaweza kupunguzwa.
Nini husababisha shinikizo la damu?
Kuna aina mbili za shinikizo la juu la damu ;
Shinikizo la juu la damu la lazima (Essential Hypertension)

Aina hii ya shinikizo la juu la damu huathiri kati ya asilimia 90-95% ya watu wanaougua shinikizo la juu la damu.Hata hivyo hakuna sababu ya kisayansi ya uhakika iliyokwisha kutolewa kuelezea kwa nini ingawa kuna baadhi ya vigezo vinaorodheshwa kuhusika na shinikizo hilo la juu la damu.
Vigezo visivyobadilika:
Umri:Kadri umri unavyoongezeka ndivyo uwezekano wa kupata shinikizo la juu la damu unavyozidi kuwa mkubwa kwa sababu kuta za mishipa ya damu huzidi kuwa ngumu hivyo kushindwa kutanuka kirahisi na kuongeza shinikizo (pressure)
Asili (Race): Jamii ya watu weusi (waafrika) wana hatari kubwa zaidi kupata shinikizo la damu kuliko watu weupe.
Histori a ya Kifamilia (Kurithi): Imegundulika kuwa uwezekano wa ndugu kupata shinikizo la juu la damu ni mkubwa iwapo ndugu wengine katika familia wamekwishawahi/wanaugua ugonjwa huo.
Jinsia:Wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata shinikizo la juu la damu kuliko wanawake.
Vigezo vinaivyobadilika:
Hivi ni vile ambavyo kwa lugha nyingine vyaweza kuepukwa.
Unene wa kupita kiasi: Unene wa kupita kiasi ni uzito wa zaidi ya “body mass index” (BMI) 30kg/m2 (BMI =uzito (kwenye kg) ÷ Urefu (kwenye mita)2 )

Kiwango cha chumvi (sodium) mwilini : Baadhi ya miili ya watu hugundua haraka kiwango cha chumvi (sodium) na shinikizo lao la damu hupanda punde watumiapo chumvi.Kupunguza matumizi ya chumvi husaidia kupunguza shinikizo la damu. Vyakula vya viwandani na madawa ya kupunguza maumivu huwa na kiasi kikubwa cha madini ya chumvi “sodium”
Vidonge vya majira: Baadhi ya wanawake wanaotumia vidonge vya uzazi wa majira hupata shinikizo la juu la damu.
Kutokufanya mazoezi: Kutokufanya mazoezi ni moja ya sababu zinazopelekea unene wa kupita kiasi (obesity).
Madawa: Baadhi ya madawa kama Amphetamines huweza kupandisha shinikizo la damu.

Shinikizo la juu la damu litokanalo na magonjwa mengine (Secondary hypertension)
Aina hii ya shinikizo huathiri karibu asilimia 10 ya watu.Hutokana na magonjwa mengone kama:
-Magonjwa sugu ya figo
-Uvimbe kwenye tezi za figo (adrenal gland)
-Kupungua kwa upana wa mshipa mkuu tuoao damu kwenye moyo kwena mwilini (coarctation of aorta)
-Ujauzito
-Matumizi ya vidonge vya majira
-Matumizi ya kupita kiasi ya pombe
-Kutokufanya kazi kwa tezi mdundumio (thyroid gland dysfunction)
-Madawa na sumu (kokeini)
Dalili za Shinikizo la Juu la Damu
Kwa kawaida Shinikizo la juu la damu huwa halionyeshi dalili na kama zikitokea basi huwa kwa kiasi kidogo na zisizo maalum na ndio maana ugonjwa huu huitwa “Muuaji wa Kimya kimya” (Silent Killer).Watu wenye Shinikizo la juu la damu huwa hawajifahamu mpaka wanapopimwa.
Baadhi ya watu wenye shinikizo la juu la damu huwa na dalili zifuatazo:
-Maumivu ya Kichwa
-Kizunguzungu
-Kutoona sawasawa
-Kichefuchefu
-Kichomi
-Kuchoka haraka
Uchunguzi na Vipimo
Kupima Shinikizo la damu kwa kutumia Mashine ya Kupimia Presha ili kujua kama ni zaidi ya Milimita za Mekyuri 140/90.
Damu: Kuangalia kiwango cha Yurea (urea),madini (electrolytes) na Krietinini (Creatinine)
Kiwango cha Mafuta (Lipid profile) kuangalia aina tofauti za lehemu (cholesterol)
Vipimo maalum vya homoni za tezi za figo (adrenalini) and tezi mdundumio (thyroid)
Mkojo kutazama madini (electrolytes) au homoni
Mionzi ya sauti (ultrasound) kutazama kama figo zimeharibika au kuvimba
Echocardiagram (ECHO) kuchunguza kama moyo umetanuka mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida kwenye mishipa ya moyo au valvu.

Viungo au mifumo iathirikayo na shinikizo la juu la damu
Mfumo was fahamu (Central Nervous System): Kuvuja kwa damu kwenye ubungo (interecerebral hemorrhage), kiharusi (stroke)

Mfumo wa kuona /macho (ophthalmologic): Kuvunja damu kutokana na kupasuka kwa mishipa midogo ya damu (fundal hemorrhages)

Moyo: Kutanuka kwa ventriko ya kushoto ya moyo (left ventricular hypetrophy) ambayo kupungua kwa kiwango cha damu kisukumwacho na moyo maumivu ya moyo (Angina Pectoris).
Mishipa ya damu: kuharibika kwa mishipa (diffuse atherosclerosis)
Figo: kudhurika kwa mishipa ya damu kwenye figo (Nephrosclerosis), kuziba kwa mishipa ya damu ipelekayo damu kwenye figo (renal artery stenosis)

Kinga
Jali uzito wako kwa kutonenepa kupita kiasi
Kufanya mazoezi pia hupunguza uzito
Punguza kiwango cha chumvi kwenye chakula
Punguza kiwango cha pombe ( si zaidi ya bia tatu (3) kwa Mwanaume na bia (2) kwa siku kwa mwanamke
Kula mlo wenye matunda na mboga za majani zaidi, samaki, maziwa, samli nk
Punguza vyakula vyenye mafuta haswa lehemu (cholesterol)
Acha kuvuta tumbaku (sigara)
Punguza msongo wa mawazo (stress) kwa kufanya mazoezi, yoga n.k

Matibabu na Ushauri
Shinikizo la juu la damu ni ugonjwa wa muda mrefu (kudumu) na ili udhibitiwe, mabadiliko katika mwenendo wa kuishi (litestyle) na matumizi sahihi na endelevu ya dawa lazima yazingatiwe.Ni muhimu kujenga utamaduni wa kupima shinikizo la damu mara kwa mara kwa sababu mara nyingine dalili huchelewa kuanza kuonekana.
Upasuaji
Upasuaji waweza kuhitajika kama kuna uvimbe katika tezi za figo (adrenal glands) ambazo zinatengeneza homoni.
Kuziba kwa mshipa upelekao damu kwenye figo (narrowing of renal artery) kunaweza kufanya upasuaji kufanyika kurekebisha tatizo.
Onana na daktari wako kama una dalili zilizotajwa hapo juu,usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari.
Dondoo za kubadili tabia
1. Tumia ngazi badala ya lifti
2. Paki gari mbali kidogo kutoka kwenye ofisi
3. Endesha baiskeli
4. Jishughlishe na bustani
5. Fanya usafi wa nyumba
6. Cheza muziki
______________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
*Si ruhusa kuinakili,kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii.Dkt. Ringo Moses, Simu:+255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com au ringomoses@gmail.com*
______________________________________________________
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 28 Oktoba 2007)