Tuesday, January 8, 2008

UGONJWA WA PUMU (ASTHMA)

Karibuni tena wapenzi wasomaji wa safu hii ya Daktari wako.Jumapili ya leo tutaangalia Ugonjwa wa pumu au asthma kama ujulikanavyo kwa lugha ya kitaalamu.

Ugonjwa huu si mgeni miongoni mwa watu wengi na ni dhahiri ama tumeshawahi kumwona au kuishi na mgonjwa wa pumu kama siyo baadhi yetu kuugua ugonjwa huu.

Utangulizi

Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu ambao huathiri njia za hewa ambazo huingiza na kutoa hewa katika mapafu.Upatapo ugonjwa wa pumu, kuta za ndani za njia ya hewa hupata maumivu (inflammation) na kuvimba.

Maumivu katika njia za hewa huzifanya kujihami kwa kusinyaa na hivyo kupunguza kiasi cha hewa kinachopita kwenda kwenye mapafu.Hali hii husababisha muathirika kutoa mlio kama wa filimbi au mluzi wakati wa kupumua.
Ugonjwa wa pumu ni ugonjwa sugu lakini unaotibika.Unaweza kudhibitiwa kama vile ugonjwa wa kisukari na moyo unavyoweza kudhibitiwa.

Aina za Pumu

Kuna aina kuu mbili za pumu.Aina ya kwanza ni ile inayoanza mapema (early onset asthma) na aina ya pili ni ile inayochelewa kuanza (late onset asthma).Kwa kifupi tutaenda kuangalia tofauti chache kati ya aina hizi za pumu.

Pumu inayoanza mapema
Ni kawaaida kwa aina hii ya pumu huanza utotoni na kwa kawaida huwatokea waathirika ambao miili yao hutengeneza kingamwili (antibodies) za IgE.Waathirika wa aina hii ya pumu hutambuliwa kwa vipimo maalum vya ngozi ambapo huonyesha kuathirika kwa asilimia kubwa ya vipimo hivyo vinapofanywa.

Pia waathirika hawa huwa na matatizo mengine ya mzio (allergic disorders) kama mafua na ukurutu (eczema)

Pumu inayochelewa kuanza
Aina hii ya pumu,tofauti na iliyopita,huanza katika umri wowote na asilimia kubwa ya waathirika ni watu wazima.Hakuna ushahidi wowote unaohusianisha vizio (allergens) vinavyotokana na mazingira na uwezo wa kusababisha aina hii ya pumu.

Pumu husababishwa na nini?

Bila shaka mpenzi msomaji umekua ukijiuliza swali hili mara kwa mara.Haifahamiki haswa ni sababu zipi zinazopelekea njia za hewa kupata maumivu na hivyo kupelekea mtu kupata pumu.Vyanzo mbali mbali vinaonyesha kuwa ni kutokana na mseto wa vitu kama tumbaku,maradhi na baadhi ya vizio.Pia kuna vitu katika mazingira ambavyo vinaweza kusababisha mtu kushambuliwa na pumu.Vitu kama vile mazoezi, vizio, viwasho (irritants) na maradhi yatokanayo na virusi.

Baadhi ya vizio ni kama vifuatavyo:
-Vumbi
-Mende
-Chavua (pollen) kutoka kwenye miti na majani
-Magamba ya wanyama,manyoya n.k

Viwasho kama:
-Moshi wa sigara
-Uchafuzi wa hewa
-Harufu kaili (kutoka kwenye rangi au chakula)
-Msongo wa mawazo

Vingine ni kama:
-Madawa kama Aspirin
-Ugonjwa wa kucheua
-Viwasho au vizio vitokanavyo na kemikali
-Magonjwa ya njia ya hewa n.k

Ieleweke kwamba orodha iliyotajwa hapo juu siyo kamilifu kwa maana kwamba haijasheheni vitu vyote vinavyoweza kuleta dalili za pumu na pia muathirika anaweza kuathirika na kimoja wapo au zaidi.

Vigezo hatarishi
Baadhi ya vigezo hatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa kusababisha ugonjwa wa pumu ni pamoja na:
-Kuishi katika miji mikubwa,haswa katikati ya mji ambapo huongeza uwezekano wa kukutana na vizio
-Kuvuta hewa iliyo na moshi
-Kemikali zitokanazo na kilimo,dawa za kutengeneza nywele, rangi, vyuma, plastiki au vifaa vya elektroniki
-Kuwa na mzazi mmoja au wawili wenye pumu
-Kuathirika na maradhi ya mfumo wa hewa kama kikohozi na mafua wakati wa utoto
-Unene wa kupita kiasi (obesity)
-Ugonjwa wa kucheua na kiungulia (Gastro esophageal reflux disease)

Dalili za Pumu

Baadhi ya dalili za kawaida za ugonjwa wa pumu ni kama zifuatazo:
-Kikohozi: Mara nyingi kikohozi cha pumu huwa kikali nyakati za usiku au alfajiri na hivyo kumfanya mwathirika kutolala vizuri
-Kutoa sauti ya mfano wa mtu anayepiga mluzi au filimbi wakati wa kupumua
-Kifua kubana: Mgonjwa husikia kama kitu kinakandamiza kifuani au wakati mwingine husikia kama mtu amemkalia kifuani.
-Kukosa hewa: Baadhi hujisikia kama hawawezi kupukmua na kukosa hewa ya kutosha inayoingia au kutoka kwenye mapafu
-Kupumua haraka haraka

Ikumbukwe kwamba si watu wote huwa na dalili zilizokwisha tajwa hapo juu na dalili zaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.
Dalili pia zaweza tofautiana ukali.Wakati mwingine dalili zaweza kuwa za wastani,za kukera tu au mbaya kiasi cha kumzuia muathirika kufanya shughuli zake za kila siku.Vile vile dalili zaweza kuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha.
Dalili pia zaweza kutofautiana kwa kipindi zinapotokea.Wengine hupata dalili mara moja tu kwa mwezi,wengine kila wiki na wengine hupata dalili kila siku.Hata hivyo iwapo muathirika atapata matibabu sahihi anaweza kuishi na dalili chache au bila dalili kabisa.

Uchunguzi

Kipimo cha muhimu katika uchunguzi iwapo mtu ameathirika na pumu ni kuangalia jinsi mapafu yanavyofanya kazi.Kipimo hicho kijulikanacho kwa lugha ya kitaalamu kama spirometry hutathmini kiasi cha hewa mtu waezacho kukitoa baada ya kuvuta hewa kwa nguvu na kwa haraka kiasi gani.
Viwango huwa chini ya kawaida iwapo njia za hewa zina maumivu na zimesinyaa.
Kipimo hiki cah spirometry pia hutumika kutathmini jinsi mgonjwa wa pumu anavyoendelea,kupata nafuu au tatizo kuongezeka.
Hata hivyo kipimo hiki ni kwa ajili ya watoto wenye zaidi ya miaka mitano na watu wazima tu.

Baadhi ya vipimo vingine vinavyoweza kiufanywa iwapo kipimo cha spirometry hakitaonyesha tatizo ni:

Kipimo cha Kizio (Allergy test)
Husadia kugundua iwapo kuna vizio mbalimbali vinavyoathiri mwili wako.

Kipimo cha Mazoezi
Kugundua iwapo kuna mabadiliko yoyote katika njia ya hewa kutokana na mazoezi.

Kipimo cha Ugonjwa wa Kucheua na Kiungulia
Kipimo hiki ni muhimu pia kutokana na uhusiana uliopo kati ya kiungulia,kucheua na ugonjwa wa pumu.

Kipimo cha Picha ya Mapafu (X-ray)
Kipimo hiki pia chaweza kuhitajika kuona iwapo kuna kitu chochote kilichoziba njia ya hewa au kama kuna maradhi yoyote katika mapafu au moyo.


Kutokana na vipimo daktari wako atapata picha ya ukali wa pumu yako na kukuanzishia tiba muafaka.

Matibabu

Kuna aina mbili za matibabu ya pumu.Moja ni ile ya dharura ili kutoa msaada au nafuu ya haraka.Dawa hizi ni zile zinazosaidia kutanua njia za hewa ambazo zimesinyaa (bronchopdilators) pia husaidia kuilainisha misuli ya njia za hewa iliyosinyaa ili iweze kutanuka na kuruhusu hewa ya kutosha kuingia.
Ni vizuri kutumia dawa za kuleta nafuu haraka punde uonapo dalili za pumu zilizooorodheshwa hapo juu.

Aina nyingine ya dawa ni zile za muda mrefu.Aina hizi za dawa hutumiwa mara kwa mara kwa kipindi kirefu kuzuia dalili za pumu na mashambulizi.Watu wenye pumu isiyoisha wanahitaji matumizi ya dawa ya muda mrefu.Kotikosteroidi za kuvuta (inhaled corticosteroids) ni nzuri kwa aina hii ya pumu.

Matibabu ya pumu kwa watoto
Watoto wenye pumu kama ilivyo kwa watu wazima wanapaswa kumwona daktari kwa matibabu.Watoto walio na umri mdogo wanahitaji uangalizi wa wazazi/walezi ili kudhibiti pumu.Watoto wenye umri mkubwa wanaweza kujifunza wenyewe jinsi ya kutumia dawa chini ya uangalizi mdogo kutoka kwa wazazi.


Matibabu ya pumu kwa watu wazima
Watu wazima wanaweza kutakiwa kupunguza au kuongeza matumizi ya dawa za pumu kutokana na maradhi mengine waliyonayo.Madawa kama ya kutibu shinikizo la juu la damu,ugonjwa unaotanua mboni ya jicho na kutatiza kuona (glaucoma),aspirini na dawa za maumivu (non steroidal anti inflammatory drugs) huingiliana na utendaji wa dawa za pumu au zenyewe kusababisha pumu.

Matibabu wakati wa ujauzito
Ni muhimu kudhibiti vyema ugonjwa wa pumu wakati wa mimba kwani iwapo utasababisha kusinyaa kwa njia ya hewa basi waweza kupelekea upungufu wa hewa ya oksijeni kwa mtoto hali ambayo ni hatari kwa mtoto.

Dawa nyingi za pumu hazina madhara kwa kichanga hivyo ni muhimu kuendelea na matibabu wakati wa mimba kuliko kuacha.

Kinga

Njia pekee ya kujikinga na pumu ni kuepuka vizio vinavyoweza kusababisha kuanza kwa dalili za pumu.Waweza fanya hivyo kwa kusafisha nymba kila wiki kupunguza vumbi,kuepuka kufanya mazoezi kwenye baridi,epuka moshi wa sigara, dhibiti ugonjwa wa kucheua na kiungulia,epuka kukaa na wanyama na epuka kuishi katika mazingira yenye hewa yenye unyevunyevu.

Ushauri

Jinsi ya kumsaidia mtoto mwenye pumu
-Mpeleke kwa daktari kwa uchunguzi wa mara kwa mara na matibabu
-Mueleweshe kuhusu pumu na jinsi ya kuidhibiti
-Mueleweshe ajue vitu vinavyoweza kusababisha yeye kupata dalili za pumu na jinsi ya kuepukana navyo
-Muepushe na moshi wa sigara kwa kutovuta sigara na kutoruhusu watu kuvuta sigara nyumbani kwako
-Tafuta jinsi ya kumpunguzia mtoto wako kukutana na vizio kama vumbi,chavua,mende n.k
-Hakikisha anatumia dawa kama inavyotakiwa
-Mhimize kufanya mazoezi ya viungo.



_________________________________________________________
©http://ringomoses.blogspot.com 2007
Si ruhusa kuinakili, kupunguza au kuongeza kitu katika makala hii au kuitumia bila ruhusa toka kwa Mwandishi wa Makala hii. Dkt. Ringo Moses, Simu: +255-713-550032 Barua pepe: ringomoses@yahoo.com, ringomoses@gmail.com
(Makala hii inapatikana pia katika Gazeti la Majira Jumapili la Tarehe 9 Desemba 2007)________________________________________________________________________

3 comments:

Unknown said...

asante dkt kwa somo zuri,kumbe maradhi mengi tunayasababisha sisi wenyewe asante ubarikiwe

Unknown said...

As ante sana
Je hakuna tiba ya asili?

Unknown said...

Nimependa somo lako ahsantee